Kujifunza ukiwa Ulingoni na Theresia Massawe
Kutana na Theresia Massawe, miongoni mwa wafanyakazi wa Ona stories, daktari na mchoraji mwenye ndoto za kujifunza kwenye upande wa masimulizi na ubunifu . Makala hii ya Ona Shule ikiwa ni muendelezo wa kuwakutanisha wanaofuatilia Onastories na wadau ndani ya jukwaa la wabobezi yaani (Expert Network) na inaangazia juu ya safari yake kitaaluma, kazi na uzoefu wake katika majukumu yake kikazi
‘Udaktari na Sanaa’
Theresia Massawe ni daktari wa binadamu kitaaluma alihitimu masomo yake Chuo kikuu cha St Joseph jijini Dar es salaam mwaka 2020. Mbali na hilo pia ni mbunifu wa picha za michoro ya rangi ambapo anatazamia siku za usoni kuunganisha ubunifu huo na teknolojia ya Uhalisa ghushi/AR ili kukiongezea thamani kipaji chake.
“Kipaji changu cha kuchora nilikigundua nikiwa bado shule ya msingi, ila nilivyojiunga na masomo ya Udaktari nilisimama kwa muda nilivyoanza mafunzo yangu ya utarajali ndipo nilirudi tena rasmi kwenye uchoraji.” Theresia.
Februari 2022 alijiunga rasmi na Ona stories fursa aliyoiona kupitia jukwaa la wabobezi (Expert network). Jukwaa ambalo linakutanisha watu mbalimbali wenye uzoefu aidha kitaaluma ama kipaji kwenye masuala ambayo Onastories inakuwa na jukumu la kuwaunganisha na fursa hizo pale tu zinapogonga hodi.
Akiwa na majukumu kama Msimamizi msaidizi wa miradi ( Projects manager associate), Theresia ameweza kujizolea uzoefu kupitia kipindi kifupi huku akijifunza maarifa mapya juu ya uongozi na kufanya kazi na wateja anaokutana nao kila mara
‘Kujifunza wakati ukiwa mchezoni’
Baada ya mafunzo yake ya utarajali akiwa kama daktari wa binadamu anakuja kukutana na kazi za kiuongozi na usimamiaji wa kazi ambazo hajawahi kuzisoma hapo awali, jambo zuri ndani ya Onastories wanayo desturi ya kujifunza, kujifunza wakati ukiwa mchezoni.
“Haikuwa rahisi kufahamu majukumu yangu kwa haraka, mwanzoni kabisa nilijisemea ninahitaji kujifunza na kuuliza zaidi lasivyo kazi zitaharibika, nilipochukua hatua, niliona kazi zikienda kidogo kidogo mpaka zinaisha huku zikiwa na ubora.” Amesema Theresia.
Project yake ya kwanza Onastories
Kwa mara ya kwanza Theresia anashiriki kazi yake ya kwanza ambayo ilikuwa ni usimamizi na uandaaji wa video za mradi wa ASPIRES TANZANIA ndani ya mikoa minne na kuelezea mafanikio ya kazi zinazofanywa na taasisi hiyo.
Kazi ya mradi huu ilimtaka kuhakikisha wanawasilisha video mbili kulingana na maelekezo waliyopewa na wateja ambao ni Aspire pamoja na kuzingatia viwango vya Onastories ili kutoa kazi ambayo ni nzuri mosi kwa mteja na pili kwa mtazamaji.
“ Siku naianza hii kazi nilikuwa najiuliza itaisha kweli, kila kilichokuwa kinnatakiwa kufanyika ilinibidi nisome kwanza nakala niliyopatiwa ili niwaongoze wale ambao tulikuwa tunawhoji, nilijiona mpya kabisa, ila tulipomaliza kufanya mahojiano na mtu wa kwanza nikaanza kuzoea.” anasema Theresia.
Licha ya changamoto, kazi hii ilikuwa na manufaa kwa ukuaji wa kimaarifa kwa Theresia kwani akiwa kama Production Manager aliweza kuongeza ujuzi hasa kwenye masuala ambayo hakuyafahamu awali, moja wapo ikiwa ni kuandika script/miswada kwa ajili ya usimamizi na uandaaji wa kazi (production) pamoja na kumuongezea ujasiri.
“ Kitu nilichojifunza kipya ni kupokea na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia mahitaji ya mteja anavyotaka, kitu kingine nimejifunza uandikaji wa ‘script writing’ lakini pia kiwango changu cha kujiamini kimeongezeka.” anasema Theresia.
Uzoefu na changamoto
Kupitia miradi ya ASPIRES na SCHOOL 2030 aliyoifanya Theresia chini ya Onastories amejikuta akijiongezea uzoefu katika mambo mengi na mapya kwenye maisha yake mojawapo likiwa ni jinsi ya kuzungumza na wateja lakini pia ufatiliaji wa taarifa wa kazi anazopewa kusimamia.
“ Katika nafasi nilizosimamia inahitaji sana kumsikiliza mteja anataka nini, ni tofauti kidogo na taaluma yangu ambapo mteja akija kwangu anategemea zaidi mimi ndio nimueleze achukue hatua gani. Huku ni kwamba mteja anakuja akiwa anafahamu fika ya kile anachokuletea hapo inabidi umsikilize ili ufate matakwa yake,”Amesema Theresia.
Funzo kwa Theresia.
Masuala matatu ya msingi ambayo Theresia anatushirikisha hasa kwenye uzoefu aliojizoelea akiwa kwenye miradi tajwa hapo awali ni:
- Hakuna kikomo cha kujifunza
“ Cha kwanza ni kwamba hakuna kikomo cha kujifunza , mi nimetoka kwenye miaka mitano ya udaktari lakini nimejikuta kwenye kitu kingine”
Hapa Theresia anatuasa zaidi kuwa ni muhimu tuwe tayari na turuhusu kupokea maarifa mapya na pia kuwasilisha kile tunachojifunza ipasavyo na pale unapo kwama hakuna budi kutafuta washauri ili wainyooshe njia yako katika kutafuta ujuzi.
Kujifunza hakuji tu kwa kuangalia upande mmoja wa maarifa bali kuwa na pande nyingi zitakazo kuongoza na vile unapojipatia muda wa kutosha kujisogeza hatua za mbele zaidi.
Katika karne ya 21 unaweza ukapata nafasi sehemu yoyote ile pale tu unapokubali kuongeza maarifa mapya.
2. Huhitaji kuwa na ujuzi, kila kitu utakipata ukiwa Onastories.
“Nilichojifunza hapa Onastories ni kwamba wewe njoo tu, ujuzi na maarifa utayapata hapa hapa…”
Hakika hakuna nafasi ya kipekee ambayo unaweza ukaipata huku ukiwa hauna hata thumni ya maarifa ya kile unachopangiwa ukiwa Onastories, lengo kubwa la jukwaa la wabobezi ni pamoja na kuwaunganisha watu wasiokuwa na ujuzi na ujuzi wasiofahamu unaweza usiifahamu teknolojia ya uhalisia ghushi (AR) ama uhalisia pepe(VR) ila ukiingia kwenye lango la Onastories na ukitoka ni unakuwa mbobezi na mwenye ufahamu wa kutosha.
Theresia anatukumbusha kuwa yeye ni daktari wa binadamu lakini sasa anajijenga zaidi na kuwa daktari msimulizi, daktari mchoraji ambaye ana shauku ya kuunganisha kipaji chake na teknolojia ya uhalisia ghushi.(Augmented Reality)
3. Utengenezajaji wa masimulizi.
Likiwa kama jambo jipya anaamini kuwa kila mtu anacho kipawa cha usimuliaji ila changamoto inakuja kama kweli una ufahamu uliojitosheleza kwenye kuandaa simulizi za kuvutia ambazo utakapoziunganisha na jambo lolote zinaweza kuwa zenye manufaa.
“Kitu kingine ni hasa usimamizi wa kazi za ‘production’ zinavyoenda, kwamba tunafanya nini pre production,production phase inakuwaje, na post production kinatakiwa nini”
Matarajio yake ndani ya Ona Stories
Imani yake zaidi imejikita kuendelea kujifunza mambo mengi yanayopatikana Onastories hususani teknolojia ya Uhalisia pepe/VR na Uhalisia ghushi/AR ili kuendelea kuwa bora zaidi huko mbeleni. Matarajio yake yakiwa ni kupata mafunzo mbali mbali yanayofanywa na ona stories pia yeye kuwashirikisha watu yale ambayo amejifunza.
Wito kwa wengine;Theresia anaamini ni mambo mengi vijana wanaweza kujifunza katika maisha lakini kubwa zaidi ni kuhusu technolojia ya Uhalisia pepe na Uhalisia ghushi ambayo kinara wake kwa Tanzania ni Onastories. Yeye kama mmoja wa waliobahatika kuwa sehemu ya wanafamilia wa Onastories ana tamani na wengine wajue kile ambacho amekiona na anaendelea kujifunza.
Jiunge sasa na Jukwaa la wabobezi (EXPERT NETWORK)
Makala hii imeandikwa na Ibrahim na Msafiri R. Ulimali