Uhalisia Pepe(VR): Tumaini la Simulizi za Kidigitali

Ona Stories
5 min readMay 28, 2022

--

Salim Mbiru (Picha na Wilfred Mikomangwa)

Salim Mbiru ni miongoni mwa zaidi ya vijana mia mbili waliojiunga na Ona Stories kupitia jukwaa la wabobezi (Expert network) lenye lengo la kuwakutanisha watu wenye taaluma, ujuzi, ubunifu kwa taasisi mbalimbali nchini Tanzania na duniani.

Kijana huyu wa kitanzania mwenye umri wa miaka 22, alipata ushawishi wa kujiunga na jukwaa hilo kutoka kwa rafiki yake ambaye alimtumia kiunganishi cha kutuma maombi.

Ni miezi 11 sasa tangu awe mwanafamilia wa Ona Stories na miezi minne tangu ahitimu masomo yake ya Stashahada ya filamu na televisheni katika chuo cha taifa cha sanaa na utamaduni Bagamoyo(TASUBA).

Mpaka sasa, Salim amefanikiwa kuonesha uwezo wake katika masuala ya ubunifu wa kusanifu kidijitali na hata kuwa miongoni mwa wataalamu wa kutengeneza filamu kwa njia ya Uhalisia Pepe yaani Virtual Reality (VR).

Wakati Salim akiwa ndio kwanza anaanza safari yake ya ajira, anakutana na kuikumbatia teknolojia mpya ya VR, ambayo hata elimu yake haikumpatia mafunzo juu ya hicho alichokutana nacho.

Uzuri wa teknolojia, kadri inavyo badilika, inawapa watu mwanya wa kubadilika nayo pia.

Lakini Uhalisia Pepe au VR ni nini haswa?

Uhalisia pepe ni nini (VR) ?

Barua pepe yaweza kuwa si jambo geni kwako-yenyewe ni sawa na barua inayotumwa kwa njia ya tarakilishi yaani ‘e-mail.’

Huku Uhalisia pepe inawasilisha mazingira yaliyo kwenye kompyuta kuonekana kama vitu au matukio halisi, na kumfanya mtumiaji kuhisi kuwa yuko kwenye mazingira hayo. Mazingira haya yanatambulika kupitia kifaa kinachojulikana kama miwani ya kuleta uhalisia (VR headset).

Florence Nkini na Salim Mburu wakiwa wamevalia miwani maalumu ya kuonyeshea filamu za uhalisia pepe (Picha kutoka Onastories)

Kadri teknolojia inavyozidi kukua na kubadilika baadhi ya mambo au kazi ambazo zilikuwa zikifanywa na binadamu kwa kutumia muda mwingi na akili, zimechukuliwa nafasi zake mfano halisi ukiwa kupotea kwa ‘typewriter’ baada ya ujio wa kompyuta.

Hii ni sawa na kusema kuwa hata uhalisia pepe nayo imeanza kuwa mbadala wa vikao, kuhadithia na katika utengenezaji wa taswira hasa kwenye upande wa usanifu majengo.

Kikao kinachofanyika kwenye uhalisia pepe. (Picha kwa hisani ya Oculus)

Upekee wake zaidi unaweza kumfanya mtu awe na uwezo wa kuangalia pande zote za dunia yaani katika nyuzi 360, ni jambo ambalo huwezi kuliona kwenye video za kawaida zilizopo kwenye mstari mnyoofu wa nyuzi 180 ambayo ni kama nusu yake.

Safari ya Salim katika Dunia ya VR

Akiwa bado mwanafunzi, Salim hakuwahi kufahamu uundaji wa filamu za uhalisia pepe (VR) mpaka alipokuwa mwanafamilia wa Onastories.

Akiwa mmoja wa waandaaji wa maudhui ya uhalisia pepe wa siku 30 walioita Dunia duara, Salim anaeleza kuwa ndio ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuifanya hiyo kazi ilimbidi atafute njia mbalimbali za kujifunza ili akamilishe kazi.

Kupitia kwenye taaluma yake ya filamu na televisheni alifundishwa uhariri unaohusisha video zilizo kwenye video katika mstari mnyoofu sasa anapokutana na hii ya uhalisia pepe uhariri wa kazi unabadilika tofauti na ule wa awali.

“Kazi ya kwanza kuandaa na kuhariri ya uhalisia pepe ilikuwa inaitwa Dunia Duara ikijumuisha video 30 kwaajili ya mitandao ya kijamii ya Onastories, ilikuwa ni ngumu wakati ninaanza kuifanya nilidhani kompyuta hazifanyi kazi kumbe ni mimi ndio sikuwa na ufundi wa kutosha kung’amua namna ya kukamilisha, lakini baadae nilifanikiwa.” Salim ameeleza.

Kwa muda wa wiki alijiwekea malengo ya kukamilisha hasa katika kuhakikisha kazi za Dunia Duara za Onastories zinakamilika kwa wakati na yeye pia kujifunza mbinu mbalimbali ili kwenda sambamba na teknolojia ya uhalisia pepe.

Safari ya Kenya na kuongeza wigo wa taaluma yake

Kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo vijana wabunifu, Ona Stories ilimpeleka Salim,jijini Nairobi nchini Kenya, kwa mafunzo ya wiki moja. Huko alikutana na wataalamu na marafiki wa Ona Stories, BlackRhinoVR wanaofanya kazi nyingi zaidi za kutengeneza video mjongefu kwenye mfumo wa uhalisia pepe.

Salim akiwa na wataalamu wa uhalisia pepe kutoka BlackRhinoVR, nchini Kenya (Picha kwa hisani)

Miongoni mwa mambo mengi aliyojifunza kuhusu VR, kuna mambo makuu matano ambayo yalikuwa mapya kwake:

  1. Kujua kutofautisha video mjongefu za nyuzi 360 na zile za mstari mnyoofu (linear).
  2. Uandaaji wa muongozo (script) ambao ni tofauti sana na miongozo inayozoeleka kwa wanaotengeneza filamu, itakuhitaji kumuangalia au kuwa kwenye viatu vya atakaye angalia na sio kumchanganya.

3. Kwa sababu ya miundo mbinu ya kamera zinazochukua pande zote kwa wakati mmoja. Hivyo muongozaji wa filamu, pamoja na kundi la waendeshaji, hawatakiwi kuonekana kwenye eneo la tukio wakati video inaporekodiwa. Simu za mkononi/ janja ndio zinatumika kuchukua video

4. Kupitia programu tumishi ya kompyuta kwaajili ya kuunganisha video mbili za nyuzi 180 (stitch) ili kukamilisha nyuzi 360.

Video mbili za nyuzi 180 zikiunganishwa ndio zinatengeneza nyuzi 360.

5. Kuondoa mstari unaotenganisha na video mbili, hii ni katika hatua ya mwisho ili kupata kazi nzuri.

Katika njia hizi zote nazo zinaainisha mambo muhimu ndani yake kama vile upangiliaji wa matukio hasa ya kile unachotaka kuchukua kwa muda huo.

Sauti: kuhakikisha inachukuliwa na aidha camera au kifaa spesheli inayoitwa (Zoom H3 VR) hii ni mahsusi kwaajili ya video za 360, ndio zinafanya sauti isikike vizuri na isiwe shida kwa atakaye kuwa anatazama kusikiliza pia.

Kingine cha kuzingatia ni kuchukua matukio wakati ambao ni wa mwanga asilia yaani kutoka kwenye jua au mwezi ila inapotokea unahitaji usaidizi wa taa basi ni muhimu kuziweka sehemu ambayo hazitaonekana.

Muandaaji wa VR anapaswa kufanya nini?

Mambo muhimu ambayo Salim anatushirikisha, kwa yoyote anayetaka kutengeneza filamu za nyuzi 360 ni muhimu kufahamu:

  • Maudhui anayotaka kuyatengeneza ni ya aina gani na hadhira ipi pia ungetamani waone kitu gani na hii inatokana na kwamba kuna aina mbili za watazamaji wa VR ambao ni;

Mtu wa kwanza ambaye ni wewe mtazamaji unakuwa kama ndio mhusika kwenye filamu, ukivaa miwani maalum ya VR unakua unaionaje kama wewe ndio mtu unaiendesha hiyo filamu (main character)

Mtu wa Tatu huyu anakuwa mtu wa nje ambaye yeye anakuwa kama mtazamaji tu.

  • Wakati ukiwa unarekodi inakupasa kamera isikuone, kwani utakapojiona kupitia kwenye simu janja jua fikra kamera nayo inakutazama na ndicho ambacho mtazamaji atakachokiona. Na inapotokea umeonekana ni aidha urudie kuchukua matukio au utengeneze video mfanano (clean plate) ili uniunganishe na ile ambayo mtu anaonekana na kumuondoa (masking out).

“ Tuko kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda na hasa kwenye upande wa teknolojia hauwezi kuiacha kuizungumzia VR kwa Tanzania ni suala la muda tu licha ya kwamba bado tupo nyuma na watu wanaoliweka kwenye macho ya watu ni Onastories, ila wataalamu wake wanapata ujuzi mkubwa basi tutegemee makubwa.”- Salim.

Imeandikwa na Msafiri R. Ulimali kwa mahojiano na Salim Mbiru.

Jiunge sasa uwe mmoja wapo wa kupata nafasi ya kuonesha ujuzi ulionao Ona Stories Expert Network.

--

--

No responses yet